Kiongozi (2/3)
Siku iliyofuata kila mtu aliyekuwa na ujasiri wa kwenda safari ndefu akakusanyika. Zaidi ya familia mia mbili walifika mahali palipochaguliwa. Ni wachache tu waliobaki nyumbani kutunza nyumba ya zamani.
Kwa kweli ilisikitisha kuona umati huu wa watu wenye huzuni ambao mkosi ulilazimisha kuacha ardhi ambayo walizaliwa na ambapo makaburi ya babu zao yamelala. Nyuso zao zilinyong’onyea, zimechakaa na kuchomwa na jua. Mateso ya miaka mingi na mirefu ya uchapakazi yalionekana kwao na ikatoa picha ya huzuni na kukata tamaa kali. Lakini mda huu palionekana mwanga wa matumaini – uliyochanganyika na hamu ya kuwa nyumbani hakika. Chozi lilitiririka kwenye nyuso zilizokunjana za wazee wengi ambao waliguna na kutikisa vichwa vyao huku wakihisi hewa mbaya ya shetani ikitabiri mabaya. Afadhali abaki kwa muda ili na yeye afe kati ya miamba hii badala ya kutafuta nchi bora. Wanawake wengi waliomboleza kwa sauti kuu na kuaga wapendwa wao waliokufa ambao makaburi wakiyaacha.
Wanaume walikuwa wakijaribu kuweka ushujaa mbele na walikuwa wakipiga kelele, – Je! Mnataka kuendelea na njaa katika nchi hii iliyolaaniwa na kuishi kwenye vibanda hivi? – Kwa kweli wangependelea zaidi kuuchukua mkoa wote uliolaaniwa pamoja nao kama inawezekana.
Kulikuwa na kelele za kawaida na kupiga kelele kama ilivyo katika kila mkusanyiko wa watu. Wanaume na wanawake hawakuwa na utulivu. Watoto walikuwa wakilalama kwenye vikoi kwenye migongo ya mama zao. Hata mifugo haikuwa na utulivu. Hapakuwa na ng’ombe wengi sana, ndama hapa na pale na kisha farasi mwembaba, mchafu mwenye kichwa kikubwa na miguu minene ambapo walikuwa wakipakia vitambaa vya zamani, mifuko na hata magunia mawili juu ya kiti cha farasi, huku mnyama huyu fukara akitapatapa kwa uzito huu. Walakini alifanikiwa kusimama na kulalama mara kwa mara. Wengine walikuwa wakipakia punda; watoto walikuwa wakivuta mbwa kwa jozi. Kuzungumza, kupiga kelele, kutukana, kuomboleza, kulia, kupiga mayowe, kulalama – yote yalijaa. Hata punda walilalama mara chache. Lakini kiongozi hakutoa hata neno, kana kwamba mambo yote hayakuwa yanamhusu. Mtu mwenye busara kweli!
Alikaa tu kwa utulivu na ukimya, na kichwa chake chini. Mara kwa mara akitema mate; ni hayo tu. Lakini kwa sababu ya tabia yake ya kushangaza, umaarufu wake uliongezeka sana hivi kwamba wote wangepitia moto na maji, kama walivyomsemea. Mazungumzo yafuatayo yanaweza kusikika:
– Tunapaswa kufurahi kupata mtu kama huyo. Laiti tungetangulia pasipo yeye, Mungu atuokoe! Tungeangamia. Ana hekima halisi, nakwambia! Yeye ni mkimya. Bado hajanena chochote! – alisema mmoja wao huku akimwangalia kiongozi kwa heshima na fahari.
– Anapaswa kusema nini? Mtu anayesema mengi hafikirii sana. Mtu mwenye busara, hakika! Anatafakari tu na kutokusema chochote, – akaongeza mwingine, na yeye pia alimwangalia kiongozi huyo kwa mshangao.
– Si rahisi kuwaongoza watu wengi! Lazima akusanye mawazo yake kwa sababu ana kazi kubwa mikononi mwake, – alisema wa kwanza tena.
Wakati ulifika wa kuanza safari. Walingoja kidogo, hata hivyo, ili kuona ikiwa kuna mtu mwingine angebadilisha mawazo yake na kuja nao, lakini kwa kuwa hakuna mtu aliyekuja, hawakuweza kuketi tena.
– Je! Hatupaswi kuondoka? – walimuuliza kiongozi.
Akainuka bila kusema neno.
Wanaume wenye ujasiri zaidi mara moja walikusanyika karibu naye ili kuwa karibu wakati wa hatari au dharura.
Kiongozi, akitikisa kichwa chake, alichukua hatua chache, akizungusha fimbo yake mbele yake mwenyewe kwa mtindo wenye hadhi. Mkutano huo ulifuata nyuma yake na kupiga kelele mara kadhaa, “Aishi kiongozi wetu muda mrefu!” Alichukua hatua kadhaa zaidi na akaingia kwenye uzio mbele ya ukumbi wa kijiji. Hapo, kwa asili, alisimama; kwa hivyo umati ukasimama pia. Kiongozi kisha akarudi kidogo na akafunga fimbo yake kwenye uzio mara kadhaa.
– Je! Unataka tufanye nini? – waliuliza.
Hakusema chochote.
– Tunapaswa kufanya nini? Tuangamize uzio huu! Hivi ndivyo tunapaswa kufanya! Je! Hauoni kuwa ametuonyesha na fimbo yake nini cha kufanya? – walipiga kelele wale waliosimama karibu na kiongozi.
– Hilo ndilo lango! Hilo ndilo lango! – walipiga kelele watoto na kuashiria lango ambalo lilikua mkabala nao.
– Ssh, kimya, watoto!
– Mungu atusaidie, nini kinaendelea? – wanawake wachache walijiuliza.
– Sio neno! Anajua la kufanya. Angamiza uzio huu!
Papo hapo uzio ulikuwa chini kama vile haukuwepo awali.
Wakaupita uzio.
Ni wazi walikuwa wamekwenda hatua mia wakati kiongozi huyo alikutana na kichaka kikubwa cha miiba na akasimama. Kwa ugumu mkubwa aliweza kujipenyeza kisha akaanza kugonga fimbo yake pande zote. Hakuna mtu aliyejigusa.
– Na ni nini sasa? – Walipiga kelele wale walio nyuma.
– Kata chaka la miiba chini! – Walisema wale waliosimama karibu na kiongozi.
– Barabara ile pale, nyuma ya vichaka vya miiba! Ile pale! – walipiga kelele watoto na hata watu wengi wa nyuma.
– Barabara ile pale! Barabara ile pale! – Aliwadhihaki wale walio karibu na kiongozi, wakiwafatiliza kwa hasira. – Je! Sisi vipofu tunawezaje kujua wapi anatuongoza? Kila mtu hawezi kutoa amri. Kiongozi anajua njia bora zaidi na ya moja kwa moja. Kata kata vichaka hivyo vya miiba!
Wakaingia ili kusafisha njia.
– Aah!, – alilia mtu ambaye alichomwa mkononi na mwiba na mtu mwingine ambaye uso wake ulichomwa na tawi la forosadi nyeusi.
– Ndugu, huwezi kuwa na kitu kwa bure. Lazima ujikakamue kidogo ili kufanikiwa, – akajibu jasiri kuliko wote kwenye kikundi.
Wakafaulu kupita kichaka baada ya juhudi nyingi na kuendelea mbele.
Baada ya kutangatanga mbele kidogo, walikuta mzigo wa magogo. Haya, pia, yakatupwa kando. Kisha wakaendelea.
Waliweza kutembea sehemu ndogo sana kwa siku ya kwanza kwani iliwabidi kukabiliana na vizuizi, kama vile. Na haya yote kwa chakula kidogo kwa sababu wengine walileta mkate mkavu tu na jibini kidogo wakati wengine walikuwa na mkate tu wa kutosheleza njaa yao. Wengine hawakuwa na chochote kabisa. Kwa bahati nzuri ilikuwa wakati wa majira wa joto hivyo walipata miti ya matunda hapa na pale.
Hata hivyo, ingawa siku ya kwanza ni sehemu ndogo tu ilibaki nyuma yao, walihisi uchovu sana. Hakuna hatari kubwa zilizotokea na hakukuwa na ajali zozote. Kwa kawaida katika shughuli kubwa kama hii matukio yafuatayo lazima yachukuliwe kuwa hayana umuhimu sana: mwiba ulichoma jicho la kushoto la mwanamke, ambalo alifunikwa na kitambaa kibichi; mtoto mmoja alipiga kelele na akajikwaa kwenye kisiki; mzee alijigonga kwenye chaka la forosadi nyeusi na kuumia kwenye kifundo cha mguu wake; baada ya kuweka vitunguu juu yake, mtu huyo alivumilia maumivu kwa ujasiri na, akiegemea kwenye fimbo yake, akachechemea na kwenda mbele kwa nguvu nyuma ya kiongozi. (Kwa kweli, baadhi ya watu walisema kwamba yule mzee alikuwa anadanganya kuhusu kifundo chake cha mguu, na alikuwa anajifanya tu kwa sababu alikuwa na hamu ya kurudi nyuma.) Punde, kulikuwa na wachache tu ambao hawakuwa na miiba mikononi mwao au mikwaruzo usoni. Wanaume walivumilia yote kwa uhodari wakati wanawake walilaani saa ile walipoondoka na watoto walilia, kwa kawaida, kwa sababu hawakuelewa taabu hii yote na maumivu itazawadiwa vizuri.
Zaidi wa furaha na faraja ya kila mtu, hakuna chochote kilichotokea kwa kiongozi. Kwa kweli, ikiwa tunasema ukweli, alikuwa analindwa sana, lakini bado, mtu huyo alikuwa na bahati nzuri. Kwenye kambi ya usiku wa kwanza kila mtu aliomba na kumshukuru Mungu kwamba safari ya siku ilifanikiwa na kwamba hakuna chochote kibaya, hamna hata mkosi mdogo vipi, ulimkuta kiongozi. Ndipo mmoja wa wanaume jasiri zaidi akaanza kuongea. Uso wake ulikuwa umekwangululiwa na kijiti cha chaka la forosadi nyeusi, lakini hakujali.
– Ndugu, – alianza, – safari ya siku moja iko nyuma yetu kwa mafanikio, asante Mungu. Barabara sio rahisi, lakini ni lazima tuishike kwa sababu sote tunajua kuwa barabara hii ngumu itatupeleka kwenye furaha. Mungu Mwenyezi na amlinde kiongozi wetu kutokana na madhara yoyote ili aendelee kutuongoza kwa mafanikio.
– Kesho nitapoteza jicho langu la pili ikiwa mambo yataenda kama leo! – mmoja wa wanawake akasema kwa hasira.
– Aah, mguu wangu! – mzee alilia, akitiwa moyo na maelezo ya yule mwanamke.
Watoto waliendelea kulia na kulia, na akina mama walikuwa na wakati mgumu wa kuwanyamazisha ili msemaji asikilizwe.
– Ndio, utapoteza jicho lako lingine, – akasema kwa hasira, – na upoteze yote mawili! Sio bahati mbaya kwa mwanamke mmoja kupoteza macho yake kwa sababu ya mchakato mkubwa kama huu. Kwa aibu! Je! Hufikirii hata juu ya ustawi wa watoto wako? Wacha nusu yetu tuangamie kwenye hii juhudi! Inafanya tofauti gani? Jicho moja ni nini? Je! Macho yako yana matumizi gani wakati kuna mtu anayetutafuta na kutuongoza kwenye furaha? Je! Tunapaswa kuachana na jitihada zetu kwa sababu ya jicho lako na mguu wa mzee?
– Anasema uwongo! Mzee anasema uongo! Anajifanya tu ili arudi, – sauti zilisikika kutoka pande zote.
– Ndugu, mtu yeyote ambaye hataki kwenda mbali zaidi, – akasema msemaji tena, – aachwe arudi badala ya kulalamika na kuchochea wengine wetu. Kwa kadiri ninavyohusika, nitamfuata kiongozi huyu mwenye busara kwa chochote kilichoachwa ndani yangu!
– Sote tutafuata! Sote tutamfuata kadri tunavyoishi!
Kiongozi alikuwa kimya.
Kila mtu alianza kumtazama na kunong’ona:
– Ametekwa na mawazo yake!
– Mtu mwenye busara!
– Angalia paji lake la uso!
– Na kila wakati kanuna!
– Bila utani!
– Yeye ni jasiri! Hiyo inaonekana katika kila kitu kumhusu.
– Unaweza kusema hivyo tena! Uzio, magogo, vizuizi – yeye hulima kuvipita yote. Yeye hugonga fimbo yake, bila kusema chochote, na lazima utakisia ana maoni gani.
Ознаке:barabara, hatima, kiongozi, kusafiri, mkoa, mtu mwenye busara, nchi, nchi ya mama, shida, shujaa, uhamiaji, umasikini, uzio, wajibu