Kiongozi (3/3)

(ukurasa uliopita)

Kama hivyo siku ya kwanza ilipita, na ikifuatiwa na siku zaidi na mafanikio kama yale. Hakuna kitu cha umuhimu mkubwa sana kilitokea, matukio ya kawaida tu: walidondoka kutanguliza vichwa kwenye shimo, kisha ndani ya bonde; walikwanguliwa kwenye visiki na kwenye vichaka vya forosadi nyeusi; walikanyaga chupa; kadhaa walivunjika mikono na miguu; wengine waliugua pigo kichwani. Lakini mateso haya yote yalivumiliwa. Wazee wachache waliachwa wamekufa kando ya barabara. “Wangekufa tu hata wangekuwa wamekaa nyumbani, bila kuja barabarani!” wasemaji walisema, wakiwatia moyo wengine kuendelea. Watoto wadogo wachache, mwaka mmoja hadi miaka miwili, pia waliangamia. Wazazi walishikiilia maumivu ya mioyo yao kwa sababu ilikuwa mapenzi ya Mungu. “Na kwa watoto wadogo zaidi, ndivyo ambavyo huzuni ilikua ndogo. Wakati wanapokuwa wachanga zaidi huzuni ni ndogo. Mungu awasaidie wazazi wasipoteze watoto wao wakati wamefikia umri wa kuoa. Ikiwa watoto wamepania sana, ni bora wafe mapema. Halafu huzuni sio kubwa sana!” wasemaji waliwatia moyo tena. Baadhi yao walifunga vitambaa kichwani na kuweka vibonyezo vya baridi kwenye michubuko yao. Wengine walibeba mikono yao kwenye vitambaa na kuining’iniza. Wote walikua wamechakaa na kukatwa. Nguo zao zilining’inia kwa michano, lakini walisonga mbele kwa furaha. Hii yote ingekuwa rahisi kuvumilia ikiwa hawakuwa wamejawa na njaa mara nyingi. Lakini ilibidi waendelee.

Siku moja, kitu muhimu kilitokea.

Kiongozi alikuwa anatembea mbele, akizungukwa na wanaume jasiri zaidi katika kundi hilo. (Wawili kati yao walikosekana, na hakuna mtu aliyejua walikuwa wapi. Ilikuwa wazi kwa wote kwamba walikuwa wamesaliti dhumuni lao na wakakimbia. Katika hafla moja msemaji alisema kitu juu ya uasi wao wa aibu. Ni wachache tu waliamini wawili hao walikuwa wamekufa njiani, lakini hawakutoa maoni yao ili wasiwashawishi wengine.) Kikundi kilichobaki kilikuwa nyuma yao. Ghafla lilionekana bonde kubwa sana na kina, kina kirefu sana hakika. Mteremko ulikuwa mkali sana kiasi kwamba hawakuthubutu kuchukua hatua moja mbele. Hata wenye ujasiri sana walisimama ghafla na kumtazama kiongozi. Akiwa amenuna, na kutekwa na mawazo kichwa chake kikiwa chini, akasogea mbele kwa ujasiri, akagonga fimbo yake mbele, kwanza kulia, kisha kushoto, kama kawaida yake. Wengi walisema haya yalimfanya aonekane mwenye heshima zaidi. Hakuangalia mtu yeyote wala kusema chochote. Kwenye uso wake hakukuwa na mabadiliko yoyote wala ishara ya hofu wakati yeye anakaribia karibu na eneo hili tupu. Hata wanaume wenye ujasiri zaidi wakawa kama kifo, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumuonya kiongozi shujaa, mwenye busara. Hatua mbili zaidi na alikuwa ukingoni. Kwa hofu kali na kwa macho kodo, wote walitetemeka. Wanaume wenye ujasiri walikuwa katika hatua ya kumrudisha kiongozi nyuma, hata ikiwa ilimaanisha kukiuka kwa nidhamu, wakati alipokanyaga mara moja, mara mbili, na kutumbukia kwenye bonde. Kukatokea mshangao, kuomboleza, kupiga mayowe; hofu ikatawala. Wengine walianza kukimbia.

– Subiri, ndugu! Je! Haraka ya nini? Je! Hivi ndivyo unavyotunza ahadi yako? Lazima tumfuate mtu huyu mwenye busara kwa sababu anajua anachokifanya. Angekuwa mwendawazimu kujiangamiza. Mbele, tumfuate! Hii ndio hatari kubwa na labda ya mwisho, shida ya mwisho. Nani anajua? Labda kwa upande mwingine wa bonde hili tutapata ardhi ya kutosha, yenye rutuba ambayo Mungu alituwekea sisi. Mbele! Bila kujitolea, hatutafika popote! – hayo yalikuwa maneno ya ushauri ya msemaji na yeye pia alichukua hatua mbili mbele, na kutoweka kwenye bonde. Jasiri zaidi walifuata na kisha kila mtu akaingia.

Kulikuwa na kuomboleza, kuugulia, kugongana, kulia kwenye mteremko wa mwinuko huu mkubwa. Mtu angekuwa akiapa kwamba hakuna mtu atakayetoka akiwa hai, bila kuumia vibaya na awe na mwili mmoja, lakini maisha ya mwanadamu ni magumu. Kiongozi alikuwa na bahati isiyo ya kawaida. Alining’inia kwenye kichaka wakati anaanguka hivyo hakuumia. Aliweza kujiondoa pamoja na kushuka. Wakati kelele, kuomboleza na kulia kumejaa chini, alikaa bila kusogea, kimya kabisa. Wachache ambao walipigwa kwa hasira walianza kumtukana lakini hakujali. Wale ambao kwa bahati nzuri waliweza kushikilia kichaka au mti wakati wa kuanguka walianza kujaribu kushuka. Wengine walikuwa wamevunjika vichwa hivyo kwamba damu ilikuwa ikiwatoka usoni mwao. Hakukuwa na mtu mwenye amani isipokuwa kiongozi. Wote walimkasirikia na kuugulia uchungu lakini hata hakuinua kichwa chake. Alikuwa kimya na kubaki kwenye mkao wa mtu mwenye busara!

Wakati ulipita. Idadi ya wasafiri ilikuwa inakuwa ndogo na ndogo. Kila siku ilichukua chake. Wengine waliacha kikundi na kurudi nyuma.

Kati ya idadi kubwa iliyoanza, ni karibu ishirini tu waliobaki. Nyuso zao, zilizochoka zilionyesha ishara za kukata tamaa, shaka, uchovu na njaa, lakini hakuna mtu alisema neno. Walikuwa kimya kama kiongozi wao na waliendelea kujivuta pamoja. Hata msemaji mwenye roho alitikisa kichwa kwa matamanio. Barabara ilikuwa ngumu kweli.

Idadi yao ilipungua kila siku hadi ikafikia kumi tu. Kwa sura zenye huzuni, waliugua na kulalamika badala ya kuongea.

Walionekana kama vilema kuliko wanaume. Wengine walikuwa kwenye magongo ya kutembelea. Wengine walishikilia mikono yao kwa vitambaa vilivyofungwa shingoni mwao. Juu ya mikono yao kulikuwa na bandeji nyingi na vigandamizio. Hata kama wangetaka kujitoa upya, hawangeweza kwa sababu miili yao haikua na nafasi ya majeraha yoyote mapya.

Hata wenye nguvu na jasiri zaidi kati yao walikuwa wameshapoteza imani na tumaini lakini bado walipambana zaidi; hivyo, walitapatapa namna fulani kwa bidii kubwa, wakilalamika, wamejaa maumivu. Nini kingine wangeweza kufanya ikiwa hawawezi kurudi nyuma? Sadaka nyingi na sasa kuachana na safari?

Kisukusuku kilishuka. Wakichechemea kwenye magongo ya kutembelea, ghafla waliona kwamba kiongozi huyo hakuwa mbele yao tena. Hatua nyingine na wote wameingia kwenye bonde lingine.

– Ah, mguu wangu! Oo, mkono wangu! – sauti zililia na kuugulia. Sauti moja dhaifu ilimlaani kiongozi anayestahili kisha alikaa kimya.

Jua lilipochomoza, hapo alikaa kiongozi, sawa na siku ile alipochaguliwa. Hakukuwa na mabadiliko yoyote  kabisa katika muonekano wake.

Msemaji akapanda nje ya bonde, akifuatiwa na wengine wawili. Wakiwa wamechakaa na wenye damu, waligeuka kuona ni wangapi wamebaki, kumbe walibaki wao tu. Hofu ya dhati na kutokuwa na tumaini vilijaza mioyo yao. Kanda hiyo haikujulikana, milima, miamba – hakuna njia mahali popote. Siku mbili kabla hawajafika barabarani lakini waliiacha nyuma. Kiongozi aliwaongoza huko.

Walifikiria juu ya marafiki na jamaa wengi ambao walikuwa wamekufa kwenye safari hii nzuri. Huzuni iliyo na nguvu kuliko maumivu kwenye miguu yao yenye ulemavu iliwashinda. Walikuwa wameshuhudia uharibifu wao wenyewe kwa macho yao wenyewe.

Msemaji akapanda kwa kiongozi huyo na kuanza kuongea kwa sauti iliyochoka, inayotetemeka iliyojaa maumivu, kukata tamaa na uchungu.

– Je! Tunakwenda wapi sasa?

Kiongozi alikuwa kimya.

– Unatupeleka wapi na umetuleta wapi? Tulijiweka sisi na familia zetu mikononi mwako na tukakufuata, tukiziacha nyumba zetu na kaburi za mababu zetu kwa matumaini kwamba tunaweza kujiokoa na dhiki katika nchi hiyo tasa. Lakini umetuharibu kwa njia mbaya zaidi. Kulikuwa na familia mia mbili nyuma yako na sasa tazama ni wangapi!

– Unamaanisha kila mtu hayuko hapa? – alinong’oneza kiongozi bila kuinua kichwa chake.

– Unawezaje kuuliza swali kama hilo? Angalia juu uone! Hesabu ni wangapi wetu tumebaki kwenye safari hii mbaya! Angalia hali ya miili yetu ilivyo! Itakuwa afadhali kufa kuliko kuwa kilema namna hii.

– Siwezi kukutazama!

– Kwa nini isiwe hivyo?

– Mimi ni kipofu.

Kimya kikatawala.

– Je! Umepoteza mtazamo wako wakati wa safari?

– Nilizaliwa kipofu!

Watatu hao waliinamisha vichwa vyao kwa kukata tamaa.

Upepo wa vuli ulipuliza vibaya kupitia milimani na kupuputisha majani yaliyokauka. Ukungu ulizunguka juu ya vilima, na kupitia baridi, ya hewa yenye unyevu ilipeperusha manyoya ya kunguru. Ndege wa mkosi alilia. Jua lilikuwa limefunikwa nyuma ya mawingu, ambayo yalikuwa yakijizungusha mbali zaidi na zaidi.

Watatu waliangaliana kila mmoja kwa mshtuko mkubwa.

– Je! Tunaweza kwenda wapi sasa?

– Hatujui!

 

Huko Belgrade, 1901
Kwa mradi wa “Radoje Domanović” uliotafsiriwa na John N. Lusingu, 2020

Ознаке: , , , , , , , , , , , ,

About Домановић

https://domanovic.wordpress.com/about/

Оставите одговор

Попуните детаље испод или притисните на иконицу да бисте се пријавили:

WordPress.com лого

Коментаришете користећи свој WordPress.com налог. Одјави се /  Промени )

Фејсбукова фотографија

Коментаришете користећи свој Facebook налог. Одјави се /  Промени )

Повезивање са %s

%d bloggers like this: