Hoja ya ng’ombe wa kawaida wa Serbia

Maajabu mengi yanafanyika katika ulimwengu huu, na nchi yetu ni, kama wengi wanavyosema, maajabu yanabubujika kwa kiwango ambacho maajabu sio maajabu tena. Kuna watu hapa kwenye nafasi za juu sana ambao hawafikirii kamwe, na kama fidia, au labda kwa sababu zingine, ng’ombe wa mkulima wa kawaida, ambaye hana tofauti hata kidogo na ng’ombe wengine wa Serbia, alianza kufikiria. Mungu anajua yaliyotokea ambayo yalimfanya mnyama huyu mwerevu kuthubutu kuchukua bidii kama hiyo, haswa kwani imethibitishwa kuwa katika kazi hii ya bahati mbaya huko Serbia inaweza kukuletea madhara. Acha basi tuseme kwamba ibilisi huyu masikini, katika kila upumbavu wake, hakujua kwamba juhudi hii haina faida katika nchi yake, kwa hivyo hatutamtaja kwa ujasiri wowote wa kiraia. Lakini bado inabakia kuwa ni fumbo kwanini ng’ombe anapaswa kufikiria wakati yeye sio mpiga kura, wala diwani, wala mzee ya kijiji, na hajachaguliwa kuwa naibu katika mkutano wowote wa wanyama jamii ya ng’ombe, au hata (ikiwa ameshafikia umri fulani) kuwa seneta. Na kama roho hii masikini ilishawahi kuota kuwa waziri wa serikali katika nchi yoyote ya jamii ya ng’ombe, angejua kwamba kinyume chake, anapaswa kufanya mazoezi ya kufikiria kidogo iwezekanavyo, kama wale mawaziri bora katika nchi zingine zenye furaha, ingawa nchi haina bahati sana katika suala hili pia. Mwishowe, kwa nini kujali ni kwanini ng’ombe huku Serbia amechukua kazi iliyoachwa na watu? Pia, inaweza ikawa kwamba alianza kufikiria tu kwa sababu ya tabia yake ya asili.

Kwa hivyo, ni ng’ombe wa aina gani? Ng’ombe wa kawaida ambaye, kama elimu ya wanyama inavyotufundisha, kichwa, mwili, na miguu, kama ng’ombe wengine wote; anavuta mkokoteni, anakula nyasi, analamba chumvi, anarudia chakula na analia kama ng’ombe. Jina lake ni Cheupe, ng’ombe wa kijivu.

Hivi ndivyo alianza kufikiria. Siku moja bwana wake alimfunga nira yeye na rafiki yake, Cheusi, walipakiza nguzo zilizoibiwa kwenye mkokoteni na kwenda nazo kuuza mjini. Karibia muda ule ule tu walipoingia mjini, aliuza zile nguzo na kisha akawafungua nira Cheupe na mwenzake, akaweka mnyororo ambao unawafungia nira, akatupa bunda la magugu mbele yao, na kwa haraka akaingia kwenye ukumbi mdogo ili kuburudika na vinywaji vichache. Kulikuwa na tafrija inayoendelea katika mji, hivyo kulikuwa na wanaume, wanawake, na watoto wakipita kutoka pande zote. Cheusi, aliyejulikana na ng’ombe wengine kama mjinga, hakuangalia kitu chochote, badala yake, alibaki kwenye chakula chake cha mchana kwa uzito wote, akala akashiba, akalia kidogo kwa kuburudika vizuri, kisha akalala, akisinzia vizuri huku anarudia chakula. Watu wote waliopita hakuwakujali vyovyote. Anasinzia na kurudia chakula kwa amani (ni huruma yeye sio mwanadamu, na utabiri huu wote wa kazi ya hali ya juu). Lakini Cheupe hakuweza kula hata kidogo. Macho yake yenye ndoto na sura ya kusikitisha ilionyesha hapo mwanzoni kwamba huyu alikuwa mtafakari, na roho tamu, isiyo na taswira. Watu, Waserbia, wanampita, wanajivunia historia yao tukufu, jina lao, taifa lao, na kiburi hiki kinaonyesha kwenye tabia yao kali na mwendo. Cheupe aliona yote haya, na roho yake ilikuwa imetekwa ghafla na huzuni na maumivu kwa sababu ya ukosefu wa haki uliokithiri, na hakuweza kuvumilia hisia kali, za ghafla na zenye nguvu; akalia kwa huzuni, kwa uchungu, machozi yakimtiririka. Na kwa uchungu wake mkubwa, Cheupe alianza kufikiria:

– Je! Bwana wangu na washirika wake, Waserbia, wanajivunia nini? Je! Kwanini wanavuta shingo zao juu sana na kuwaangalia watu wangu kwa kiburi na dharau? Wanajivunia nchi yao, wanajivunia kwamba huruma ya hatima imewajalia kuzaliwa hapa Serbia. Mama yangu alinizaa hapa Serbia pia, na Serbia sio ardhi yangu tu bali ni ya baba yangu pia, na babu zangu, kama vile wa kwao, wote kwa pamoja, walikuja katika nchi hii kutoka nchi yao ya zamani ya Slavic. Na bado hakuna mmoja wetu ng’ombe aliyejisikia fahari juu yake, sisi tu tulijivunia uwezo wetu wa kuvuta mzigo mzito kwenye kilima; hadi leo, ng’ombe hajawahi kumwambia ng’ombe mmoja wa Ujerumani: “Unataka nini kutoka kwangu, mimi ni ng’ombe wa Serbia, nchi yangu ni nchi yenye fahari ya Serbia, mababu zangu wote walikua na walizaliwa hapa, na hapa, katika nchi hii, ni kaburi za mababu zangu.” Mungu wangu, hatujawahi kujivunia hili, haijawahi kukumbukwa, na wanajivunia hata hivyo. Watu wa ajabu!

Akiwa amechukuliwa na mawazo haya, ng’ombe huyo alitikisa kichwa kwa huzuni, kengele shingoni mwake ikililia na nira likitoa sauti ya kukatika. Cheusi alifumbua macho yake, akamtazama rafiki yake, na akalia akapiga kelele:

– Haya umeanza tena na huo ujinga wako! Kula, mjinga, ongeza mafuta, angalia mbavu zako zote zilivyochomoza; kama ni vema kufikiria, watu wasingetuachia sisi ng’ombe. Hakuna njia ambayo tungekua na bahati nzuri!

Cheupe alimwangalia yule mwenzake kwa huruma, akageuza kichwa chake kutoka kwake, na kuzama tena katika mawazo yake.

– Wanajivunia zamani zao tukufu. Wana uwanja wao wa Kosovo, Vita ya Kosovo. Kubwa sana, babu zangu hawakuvuta mikokoteni yenye chakula na silaha huko nyuma? Kama isingekua sisi, watu wangelazimika kufanya hivyo wenyewe. Halafu kuna ghasia dhidi ya Waturuki. Jaribio kubwa, bora, lakini ni nani alikuwa hapo wakati huo? Ilikuwa ni hawa wajinga wenye pua za juu, wakitembea kwa kiburi mbele yangu kana kwamba ni ushindi wao, ni nani aliyeinua mapinduzi? Hapa, chukua bwana wangu kama mfano. Yeye pia anajivuna na kutamba juu ya mapinduzi, haswa na ukweli kwamba babu yake mkubwa aliangamia kwenye vita ya ukombozi kama shujaa wa kweli. Na hii ni sifa ya bwana wangu? Babu yake mkubwa alikuwa na haki ya kujivuna, lakini sio yeye; babu yake mkubwa alikufa ili bwana wangu, ukoo wake, wawe huru. Kwa hivyo yuko huru, na anatumiaje uhuru wake? Anaiba nguzo za watu wengine, anakaa kwenye mkokoteni, na inabidi nimvute yeye na hizo nguzo wakati amelala kwenye chaga. Sasa ameuza nguzo zake, anakunywa mvinyo, hafanyi chochote na anajivunia historia yake tukufu. Na ni wangapi wa mababu zangu waliouawa kwenye uasi huo kuwalisha wapiganaji? Na je! Babu zangu wakati huo hawakuvuta silaha, mizinga, chakula, risasi? Na bado hatujivunii sifa zao kwa sababu hatujabadilika; bado tunafanya kazi zetu hadi leo, kama tu mababu zetu walivyofanya, kwa uvumilivu na uangalifu.

Wanajivunia mateso ya mababu zao na ya miaka mia tano ya utumwa. Ndugu zangu wameteseka katika maisha yetu wote, na leo bado tunateseka na tumetumikishwa, na bado hatujapiga kelele juu ya sauti zetu zote. Wanasema kwamba Waturuki waliwatesa, kuwachinja na kuwachoma; vema, mababu zangu waliuwawa na Waserbia na Waturuki pia, na kukaangwa, na kuvikwa kila aina ya mateso.

Wanajivunia dini yao, na bado hawaamini chochote. Je! Ni nini mimi na watu wangu kwamba hatuwezi kukubalika kati ya Wakristo? Dini yao huwaambia “usiibe” na kuna bwana wangu anaiba na kunywa kwa pesa alizopata kwa kuiba. Dini yao huwaamuru wawapende majirani zao, na bado wanaumizana wenyewe kwa wenyewe. Kwao, wanaume bora, mfano wa fadhila, ndiye asiyefanya ubaya wowote, na kwa kweli, hakuna mtu anayezingatia kumuuliza mtu yeyote kufanya jambo zuri pia, aisipokua usitende mabaya. Hicho ndicho kiwango cha chini cha mifano yao ya wema ujazo wa zaidi ya kitu kisichokua na umuhimu ambacho hakifanyi mabaya.

Ng’ombe akapumua kwa nguvu, na kupumua kwake kukainua mavumbi barabarani.

– Kwa hivyo – ng’ombe aliendelea na mawazo yake ya kusikitisha – katika hali hii, si mimi na jamaa yangu ni bora katika yote hayo kuliko wao? Sijawahi kumuua mtu yeyote, sijawahi kumchafua mtu yeyote, sijawahi kuiba chochote, sijafukuza mtu asiye na hatia kutoka kwenye huduma ya umma, sijafanya upungufu katika hazina ya serikali, sijatangaza kufilisika bandia, Sijawahi kufunga au kuwakamata watu wasio na hatia, sijawahi kuwatukana marafiki wangu, sijawahi kwenda kinyume na kanuni zangu za ng’ombe, sijatoa ushahidi wa uongo, sikuwahi kuwa waziri wa serikali na kamwe sikuifanyia nchi yangu madhara yoyote, na sio kuwa sikufanya ubaya wowote, mimi pia huwafanyia wema wale wanaonitenda vibaya. Mama yangu alinizaa, na mara, watu wabaya hata walichukua maziwa ya mama yangu kwangu. Mungu angalau ameunda nyasi kwa ajili yetu ng’ombe, na sio kwa wanadamu, na bado wanatunyima pia. Bado, mbali na kipigo chote kile, tunavuta mikokoteni ya wanadamu, tunalima shamba zao na tunawalisha mkate. Na bado hakuna mtu anayekiri uhalali wetu ambao tunafanya kwa nchi…

– Au chukua kufunga kama mfano; vizuri, kwa binadamu, dini inasema kwamba tufunge wakati wote wa sikukuu, na bado hawako tayari kuvumilia mfungo mdogo huu, wakati mimi na watu wangu tunafunga maisha yetu yote, tangu sisi tumekomeshwa kutoka kwenye matiti ya mama zetu.

Ng’ombe aliinamisha kichwa chake kana kwamba alikuwa na wasiwasi, kisha akakiinua tena, akatoa sauti puani kwa hasira, na ilionekana kuwa kitu cha maana kilikuwa kinarudi kwake, kumnyanyasa; ghafla, akapiga kelele kwa furaha:

– Ah, najua sasa, lazima iwe hivyo – na aliendelea kufikiria, – ndivyo ilivyo; wanajivunia uhuru wao na haki za raia. Nahitaji kuliweka akilini mwangu kwa umakini.

Na alikuwa akifikiria, na kufikiria, lakini hakuweza kuvumbua.

– Je! Ni haki gani hizi za kwao? Ikiwa polisi wataamuru wapige kura, watapiga kura, na kama hivyo, tunaweza kwa urahisi kupiga kelele: „Kwa-a-ke-eee!“ Na ikiwa hawajaamriswa, hawathubutu kupiga kura, au hata kujihusisha na siasa. kama sisi. Vile vile wanapigwa gerezani, hata ikiwa hawana hatia kabisa. Angalau tunalia na kuzungusha mikia yetu, na hawana hata huo ujasiri mdogo wa raia.

Na wakati huo, bwana wake alitoka kwenye chumba cha pombe. Amelewa, anatapatapa, macho yenye ukungu, akiongea maneno kadhaa yasiyoeleweka, akatapatapa akitembea kuelekea kwenye mkokoteni.

– Angalia tu, ni vipi huyu jamaa mwenye kiburi anatumia uhuru uliopatikana na damu ya mababu zake? Sawa, bwana wangu ni mlevi na mwizi, lakini wengine hutumiaje uhuru huu? Ili tu kuzubaa na kujivunia zamani na kwa sifa ya babu zao, ambazo wamechangia sana kama mimi. Na sisi ng’ombe, tulibaki kuwa wachapakazi na wenye umuhimu kama babu zetu walivyokuwa. Sisi ni ng’ombe, lakini bado tunaweza kujivunia kazi zetu ngumu na mafanikio leo.

Ng’ombe akaguna kwa undani na kuweka shingo yake kwenye nira.

 

Huko Belgrade, 1902
Kwa mradi wa “Radoje Domanović” uliotafsiriwa na John N. Lusingu, 2020

Ознаке: , , , , , , , , , , , , , , , , , , , , , ,

About Домановић

https://domanovic.wordpress.com/about/

Оставите одговор

Попуните детаље испод или притисните на иконицу да бисте се пријавили:

WordPress.com лого

Коментаришете користећи свој WordPress.com налог. Одјави се /  Промени )

Фејсбукова фотографија

Коментаришете користећи свој Facebook налог. Одјави се /  Промени )

Повезивање са %s

%d bloggers like this: